Kwa zaidi ya siku mbili sasa kumekuwa na video za mchungaji wa kanisa la Mlima wa Moto, Dkt. Gertrude Rwakatale akiwaombea waumini wake wa kike wapate wanaume wa kuwaoa huku akitamka neno ‘Upepo wa Kisuli suli’ jambo ambalo kila mtu amekuwa na tafsiri tofauti tofauti ya maana halisi ya upepo huo.

Kufuatia tafsiri hizo, Msanifu Mkuu wa lugha kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Consolata Mushi, ameeleza maana halisi ya neno hilo ukiachana na ile ya kiimani, kupitia Kamusi sanifu ya Kiswahili Fasaha.

Bi. Consolata amesema ”Muktadha wa neno kisulisuli nikiangalia ni kwenye masuala ya imani, kumbukeni masuala ya imani kwao ni kusadiki jambo ambalo hujaliona na kuliamini kwamba litatokana kama lilivyo kwa mujibu wa msamiati wa Kiswahili, neno Kisulisuli lina maana ya upepo unaosafiri na kuzunguka na kwenda kwa kasi au kwa haraka”.

Kuhusu kauli ya Mama Rwakatare, Bi. Consolata  amesema neno hilo katika muktadha wake alimaanisha kwamba ni jambo ambalo litatokea kama kimbunga kwa sababu upepo wa aina hiyo hutokea ghafla.

“Kama yeye alitumia kama mchumba anaweza akaja kama upepo wa kisulisuli ni muktadha wa imani, kwamba wapo na watajitokeza bila kutarajia, sasa msije mkaiingiza kwamba atajitokeza anazunguka kama upepo Laa! hasha! muktadha uongozwe kwenye kupata maana ya maneno, kwamba umekwenda kanisani ni msichana ama mvulana bila mwenzio lakini pale baada ya sala na imani akatokea mwenzio hukutarajia, hukupanga,” amesema Bi. Consolata.

Aidha kwenye mitandao ya kijamii kumesambaa video pamoja na picha mbalimbali zikionesha upepo huo wa kisuli suli pamoja na utani mwingi ambao unaonesha baadhi ya ndoa zilitokana na upepo wa Kisuli Suli.

Mcheleshaji maarufu hapa nchini Mc. Pilipili amekuwa nambari moja kushare baadhi ya picha na video alizoambatanisha maneno kadhaa juu ya upepo wa Kisulisuli.

Muuguzi asakwa kwa kumbaka mgonjwa saa 4 hadi saa 8 na kutoroka
Kizaazaa: Kompyuta zenye kesi za wahujumi uchumi zaibiwa ofisini kwa DPP