Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeunga mkono marudio ya uchaguzi wa Zanzibar uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), utakaofanyika Machi 20 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum  alisema kuwa Bakwata inatoa wito kwa vyama vyote vya siasa kushiriki marudio ya uchaguzi huo ili kumpata kiongozi wao Zanzibar kwa njia za Kidemokrasia.

Aidha, Sheikh Mussa Salum aliutaka uongozi wa Chama Cha Wananchi (CUF) kutosusia uchaguzi huo na kushiriki kwa kuwa ndio njia pekee ya kupata suluhu ya uchaguzi huo kwa njia za kidemokrasia.

Pia, aliwataka ZEC kuhakikisha wanatenda haki katika kusimamia uchaguzi huo wa marudio bila kupendelea au kuonea chama chochote cha siasa.

ZEC ilitangaza Machi 20 kuwa siku ya marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar baada ya kutangaza kuufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana wakieleza kuwa uligubikwa na kasoro mbalimbali.

Mwakyembe, Mdee watunishiana misuli kuhusu Kashfa ya Mabehewa Mabovu
Baada ya Mbunge wa CCM kutaka Bangi ihalalishwe, Daktari aeleza faida na hasara zake kiafya