Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) ambaye jina lake lilitajwa mara nyingi baada ya kuibua bungeni sakata la uchotwaji wa fedha kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow, David Kafulila ameibuka tena baada ya Tanesco kuamriwa kulipa zaidi ya shilingi bilioni 320.

Baraza la Usuluhishi la Kimataifa la Uwekezaji lililokuwa likishughulikia mgogoro huo, liliamua kuwa Tanesco wailipe Benki ya Standard Chartered-Hong Kong (SCB-HK) kiasi hicho cha fedha ambacho hata hivyo hakipo baada ya kutolewa kwenye akaunti ya ‘Tegeta Escrow’ iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu na baadhi ya vigogo kugawana kupitia mabenki kadhaa nchini.

Kafulila amesema kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inapaswa kuweka wazi ripoti yake ya uchunguzi ili iweze kuwaweka wazi waliokuwa nyuma ya uchotwaji huo wa fedha.

“Leo vinara waliokuwa wakitetea IPTL bado ni vinara katika Serikali ya Magufuli, fedha za escrow hazikuwa za IPTL sasa tunaingia gharama nyingine, Shilingi bilioni 300, ni lazima tufahamu nani yuko nyuma ya mzimu huu wa escrow,” alisema.

Kadhalika, Kafulila alitaka maazimio yote ya Bunge yaliyofikiwa baada ya Kamati Maalum iliyokuwa chini ya Zitto Kabwe kuwasilisha ripoti yake, yafanyiwe kazi kwani fedha hizo lazima zitalipwa na Serikali kama ilivyokuwa kwa fedha za Dowans.

Kafulila ametaka vyombo husika kufuatiliwa chanzo cha kutolewa fedha hizo kwa uharaka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow wakati mgogoro ulikuwa unaendelea kusuluhishwa.  Amelitaka Bunge la 11 kuhakikisha linahoji na kusimamia

“Inaumiza sana kwa sababu kodi ya wananchi italipa fedha ambazo zingetumika kutatua matatizo ya wananchi katika kilimo, maji, elimu na maeneo mengine,” Kafulila anakaririwa.

Kauli ya Kafulila imekuja muda mfupi baada ya Zitto Kabwe kumshauri Rais Magufuli kuchukua hatua za haraka na kuwafikisha mahakamani wale wote wanaohusika katika sakata la Escrow.

 

Pep Guardiola: Yaya Toure Hatocheza Tena Man City
Ajali ya basi yaua 12 Njombe.