Mshambuliaji wa mabingwa wa Kenya Gor Mahia Juma Balinya amesema sababu kubwa iliyomfanya aondoke Young Africans, wakati wa dirisha dogo la usajili imetokana na imani ndogo iliyokua imejengeka kwa mashabiki wa klabu hiyo ya jijini Dar es salam.

Balinya aliomba mkataba wake na Young Africans uvunjwe mwezi Januari, baada ya kushindwa kutamba, kwenye kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria, tofauti na alivyokua akifanya nchini kwao Uganda akiwa na kikosi cha Police FC, kabla ya kutua Jangwani mwanzoni mwa msimu huu 2019/20.

“Nilitamani kuendelea kubaki Yanga licha ya changamoto zilizokuwepo lakini sikuweza kwani mashabiki hawakunikubali. Mchezaji ni rafiki wa mashabiki kama, hawakubali kazi yako huwezi kujisikia faraja,” alisema Balinya.

Baada ya kuachana na Young Africans, Balinya alisajiliwa na klabu ya Gor Mahia ambapo alifanikiwa kufunga mabao mawili katika mchezo wake wa kwanza ligi kuu ya Kenya.

Mpaka ligi inasimama kutokana na janga la Corona huko Kenya, Balinya alikuwa amefunga mabao matatu.

Katika hatua nyingine mshambuliaji huyo amesema yuko mbioni kuondoka Gor Mahia akiwa amepata ofa kutoka klabu ya Polokwane inayoshiriki ligi kuu ya Afrika Kusini.

Gor Mahia inakabiliwa na changamoto ya ukata, wachezaji wengi wakidai mishahara ya hadi miezi minne.

Haji Manara: Tupo tayari kumkabidhi kombe Rais Magufuli
Waandishi wa Kenya wakamatwa Arusha