Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amekutana na kumuaga Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada ambaye amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Ibuge amemtakia maisha mema na kumsihi kuwa balozi mwema kwa Tanzania nchini Nigeria na kwingineko duniani.

Balozi Ibuge amesema kuwa Nigeria imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta za usafirishaji, utalii, biashara na uwekezaji na usafirishaji.

Brigedia Ibuge amemhakikishia Balozi Gada, kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Nigeria, utaendelea kuimarika ikiwa ni ishara ya kuwaenzi waasisi wa mataifa ya Tanzania Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Rais wa kwanza wa Nigeria Nnamdi Azikiwe, ambapo viongozi hawa walikuwa ni sehemu ya juhudi za kukomboa bara la Afrika na hata kusimi mwa Afrika.

Brigedia Ibuge amesisitiza kuwa Tanzania na Nigeria, zitaendelea kushirikiana katika sekta ya uwekezaji na biashara kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili ambapo piaametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nchini Nigeria, kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za benki na utalii.

Kwa upande wake, Balozi Sherlock ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano iliyompatia wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na imara tangu miaka ya 1962.

Bweni la shule ya Sekondari Uchira Islamic lateketea kwa moto
Zlatko kuishtaki Yanga FIFA