Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amemuaga balozi wa Iran nchini, Mousa Ahmed Farhang ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi.

Akiongea katika hafla ya kumuaga balozi wa Iran iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi amempongeza Balozi Farhang kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi yake na Tanzania.

Prof. Kabudi amemuahidi balozi Farhang, kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Iran katika sekta za elimu, afya na utalii kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.

“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania nakuahidi ushirikiano kutoka kwetu, nakutakia kila la kheri katika maisha yako nje ya Tanzania na ni imani yangu kuwa utakuwa balozi mzuri wa Tanzania duniani,” amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Balozi Farhang ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi ambapo ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo, baina ya Iran na Tanzania katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Callum Wilson arudishwa Ligi Kuu England
Wasanii waliopata ajali kugharamiwa na CCM