Kiungo kutoka DR Congo Yannick Bangala ataukosa mchezo wa mzunguuko wa saba wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya Kwanza FC, utakaochezwa mapema juma lijalo.

Mbeya Kwanza FC inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Young Africans siku ya Jumanne (Novemba 30) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.

Bangala ambaye ameonekana kuwa mwiba katika safu ya kiungo tangu alipoanza kuitumikia Young Africans mwanzoni mwa msimu huu, ataukosa mchezo huo, kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Kiungo huyo anayecheza kwa nguvu na akili wakati wote, alionyeshwa kadi ya njano katika mchezo wa mzunguuko wa sita dhidi ya Namungo FC, mwishoni mwa juma lililopita mjini Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu.

Katika mchezo huo Young Africans ililazimisha matokeo ya sare ya bao 1-1, kwa mkwaju wa Penati uliopigwa na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saidi Ntibazonkiza.

Hata hivyo Kocha Mkuu wa Young Africans Nesreddine Mohamed Nabi amesema bado wana watu wa kuziba pengo la Bangala, kwani wanahitaji ushindi kwa nguvu zote, katika mchezo huo.

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 16, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 14, huku Mbeya Kwanza FC itakayocheza dhidi ya vinara hao ikiwa nafasi ya nane ikiwa na alama 7.

Mbeya Kwanza FC ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu mwishoni mwa juma lililopita, kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons waliokua nyumbani Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Red Arrows kutua Dar leo
Hererimana: Tunajipanga kuifunga Young Africans