Ubovu wa barabara na kutokuwepo kwa Reli kutoka Mpanda kwenda Bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi imetajwa kuwa sababu ya Bandari hiyo kuzorota kinyume na matarajio.

Akizungumza mara baada ya kuzuru mradi huo wa kimkakati, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa, amesema tangu ilipofunguliwa rasmi Septemba 2022, bandari hiyo imeingiza kiasi cha shilingi milioni nne na laki nane pekee, ambazo ni kiasi kidogo ukilinganisha na uwekezaji uliofanyika wa shilingi Bilioni 47.97.

Amesema, “tatizo kubwa la Bandari ile ni barabara, mizigo kufika na kutoka pale, barabara na reli, iko reli ya Kati unafika mpaka Mpanda na umbali wa kilomita 130 kufika mpaka Karema ambazo hazijajengwa na wakati wote serikali imekuwa ikilisemea jambo hili.”

Aidha, Silaa ameongeza kuwa, “Barabara tuliyoenda, kufika hata gari ndogo ni tabu, Bandari ile inaweza ikapunguza msongamano Tunduma. Leo mizigo ya Congo (DRC) malori yanatumia siku 45 maana yavuke Tunduma, yaingie Zambia, yaende tena yakavuke kweye mpaka mwingine wa Zambia ndio yanaingia Congo – DRC.”

Hata hivyo, amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo itasaidia malori yanayopeleka mizigo DRC badala ya kupitia Tunduma yatapitia Mpanda hadi Karema na baada ya kufika Bandari ya Karema ni rahisi kufika Bandari ya Karemii iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na baadaye Lubumbashi, jimbo kubwa la kibiashara nchini humo.

“Mpango wa serikali uliopo sasa ni kujenga barabara ya kilomita 110 kutoka Kijiji cha Kagwira hadi bandari ya Karema pamoja na kujenga reli kutoka Mpanda hadi Karema,” amesema Silaa.

Ujenzi wa mradi wa Bandari ya Karema uliogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 47.97, ulianza kutekelezwa Oktoba 2019 na kukamilika mei 2022 na kuanza kazi rasmi Septemba 2022 ukitarajiwa kuwa kitovu cha biashara kati ya Tanzania na DRC kupitia ziwa Tanganyika.

Miradi afya ya macho kugharimu Bilioni 1.47
Jishindie Tsh 800,000/= ya Expanse Casino Meridianbet