Kocha Mkuu wa Biashara United Mara Francis Baraza, amewapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri walioifanya ndani ya dakika 90 za mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliowakutanisha na Mabingwa watetezi Simba SC jana Alhamis, kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma, Mara.  

Licha ya kushuhudia kikosi chake kikipoteza mchezo huo uliokua na upinzani mkali kwa dakika zote 90, kocha Baraza aliwaambia waandishi wa habari kuwa, licha ya kufungwa bao 0-1, bado aliridhishwa na uwezo wa timu yake kwa namna ilivyocheza.

Kocha huyo kutoka nchini Kenya alisema wachezaji wake walijitahidi kupambana na kusaka bao la kusawazisha lakini bahati haikuwa kwao, huku akisisitiza kuwa wamefungwa na timu bora.

“Tumepoteza mbele ya Simba SC hilo lipo wazi ila wachezaji wangu wamecheza vizuri na wameonyesha kwamba wapo fiti asilimia 100.”

“Ndani ya uwanja walikuwa hawajidondoshi wamecheza kwa utulivu na kwa nidhamu hivyo kwa sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi zetu zijazo.” Alisema Baraza.

Ushindi huo unaifanya Simba SC kufikisha jumla ya alama 42 ikidaiwa alama nne na Young Africans inayoendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu na alama zao 46 baada ya kucheza michezo 20, huku Simba ikiwa imecheza michezo 18.

Biashara United ya Mara imeendelea kusalia kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imecheza0 jumla ya michezo 20 na kufikisha alama 32.

Mfungaji Bora - Dube arudisha matumaini
PICHA: Simba SC yarejea Dar, kuisukia mtego Al Ahly