Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Barbara Gonzales ameushauri Uongozi wa Young Africans kwa kuutaka ujifunge kibwebwe katika maandalizi ya kuelekea mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya awali dhidi ya Rivers United.

Barbara ametoa ushauri huo, baada ya kupata uzoefu wa kutosha kwenye michuano hiyo msimu uliopita, ambapo Simba SC ilianzia nchini Nigeria kwa kucheza dhidi ya Plateau United, ambapo ilichomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na Clatous Chama.

Kiongozi huyo amesema Uongozi wa Young Africans unapaswa kufuata utaratibu wa kujihami wakati wote wa kuelekea mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya wenyeji wao Rivers United, utakaopigwa Jumapili (Septamba 19), Uwanja wa Yakubu Gowon, mjini Port Harcourt katika jimbo la Rivers.

Barbara amesema kuna mambo mengi sana ya kuzingatia pindi mjumbe wa Young Africans atakapokua nchini Nigeria, huku akisisitiza mjumbe huyo awe tayari kwa kuona mambo tofauti atakayothibitishiwa na maafisa wa idara zote nchini Nigeria, hivyo asiwaamini kwa asilimia 100.

“Wajipange sawa sawa kwa sababu ugenini kuna mambo mengi hasa kipindi hiki cha Covid 19, atakaetangulia kule awe makini sana,”

“Maafisa wa idara zote wanaweza kukuaminisha kila kitu kipo vizuri, lakini siku maalum ikifika unaona mambo yanageuka ili kukutoweni kwenye mchezo, kama hawatokua imara watapoteza mchezo kwa mara ya pili.” amesema Barbara.

Tayari Uongozi wa klabu ya Young Africans umeanza maandalizi ya kuelekea mchezo wa mkondo wa pili, wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United, utakaopigwa Jumapili (septemba 19) nchini Nigeria.

Young Africans matumaini kibao
Korea Kaskazini yafanya majaribio ya makombora mapya