Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Barabra Gonzalez amesema watachukua tahadhari kubwa watakapofika Afrika Kusini, kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates.

Simba SC ilishinda bao 1-0 juzi Jumapili (April 17) dhidi ya Orlando Pirates, Uwanja wa Benjamin Mkapa na mwishoni mwa juma hili itacheza ugenini Afrika Kusini Jumapili (April 24).

Barbara amesema Uongozi wa Simba SC unatambua mchezo wa Mkondo wa Pili utakua mgumu, sambamba na kuzunguukwa na mazingira ambayo hayatakua rafiki kwa timu yao, hivyo ni lazima wajipange kuyaepuka ama kuyakwepa watakapokua ugenini.

“Mchezo wetu wa marudiano kule Afrika Kusini utakua mgumu sana, tunajua soka la Afrika lina mazingira magumu, hivyo tutajitahidi kuchukua tahadhari kubwa tutakapokuwa Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wetu na Orlando Pirates.”

“Ni jukumu letu kama viongozi kuhakikisha kila hatua tutakayoipitia tukiwa ugenini inafuata mpango tuliojiwekea na hii ni kwa ajili ya wachezaji wetu ambao wana jukumu la kuhakikisha wanapata matokeo yatakayotuvusha kwenda Nusu Fainali.” amesema Barbara

Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa 1-0, ama kusaka ushindi zaidi katika mchezo wa Mkondo wa pili ugenini Afrika Kusini siku ya Jumapili (April 24), ili kupata tiketi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kwa upande wa Orlando Pirates italazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuelendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

AVAR ajibu tuhuma za Kocha wa Orlando Pirates
Fursa za 'The Royal Tour' zatajwa