Kocha Mohamed Abdallah ‘Bares’ amethibitisha kuanza kazi Tanzania Prisons baada ya kumalizana na Uongozi wa Klabu hiyo yenye maskani yake makuu jijini Mbeya.

Tanzania Prisons imemuajiri Kocha huyo kutoka visiwani Zanzibar, baada ya Kocha Patrick Oshiambo kumaliza mkataba wake, huku akiiacha timu hiyo pabaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Bares amesema rasmi anaanza kazi ya kukinoa kikosi cha Tanzania Prisons, baada ya kumaliza mchezo wa Kombe la Shiriksiho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Mashujaa FC.

Amesema anatambua ana kazi kubwa ya kuhakikisha Tanzania Prisons inabaki Ligi Kuu, lakini atajitahidi kufanya hivyo kutokana na kuwafahamu wachezaji wengi wa klabu hiyo.

“Tayari nimeshajiunga na timu na kukabidhiwa kila kitu, majukumu yangu rasmi yataanza mara baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, mipango ni kuhakikisha naisaidia timu kufanya vizuri kwenye michezo iliyobaki ili iweze kubali Ligi Kuu.”

“Naifahamu Prisons ni timu niliyofanya nayo kazi muda mrefu, natambua uwezo wachezaji wengi waliopo, kwani hakuna mabadiliko makubwa naamini watashirikiana nami kuhakikisha tunaibakiza timu msimu huu,” amesema Bares

Tanzania Prisons ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 21 na Bares anatarajia kuanza majukumu yake rasmi kwenye mchezo wa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar.

Vyama vya upinzani, wananchi wasusia uchaguzi
Simba SC inautaka ubingwa 2022/23