Mwimbaji na mwandishi mahiri wa nyimbo za bongo flava, Barnaba Classic ambaye ndiye mwandishi wa wimbo ‘Yule’ wa Ruby amesema awali aliugawa kwa mastaa wakaukataa.

Barnaba ameiambia The Playlist ya 100.5 Times FM leo kuwa awali aliuandika wimbo huo kwa ajili ya msanii mmoja mkubwa lakini alipompa aligoma kuupokea akidai kuwa umekaa kama wimbo wa injili (gospel).

“Siwezi kumtaja jina, lakini alinambia wimbo huo hauendani naye kwa sababu anaona umekaa kama wimbo wa gospel, kwahiyo ikabidi nimpe mwingine ambaye pia aliukataa na mwisho nikampa Ruby,” Barnaba alifunguka.

Aliongeza kuwa Ruby pia aliupokea kwa shingo upande akitoa sababu kama za wasanii walioukataa, lakini baada ya kumshawishi alikubali kuufanya.

“Baada ya kutoka alinipigia simu akaniambia ‘siamini naona napokea simu za watu wengi wanaukubali’. Ndio Yule ukawa wimbo mkubwa,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Barnaba ambaye hivi karibuni ameachia wimbo wake mkubwa ‘Lover Boy’ amesema kuwa video ya wimbo huo ambayo imeanza kuoneshwa hapa nyumbani, itatambulishwa ‘exclusively’ kwenye vituo vikubwa vitatu vya kimataifa ambavyo alidai atavitaja kama surprise baadae.

Aliongeza kuwa kwa kiwango alichofika na uwezo alionao anajiona kuwa tayari ni msanii wa Kimataifa na kwamba muda ndio utakaoongea.

Barnaba ameandika nyimbo nyingi za wasanii wa Bongo Flava kama ‘Siri’ ya Vanessa Mdee, Say My Name ya Shilole, Yule ya Ruby.

Audio: 'Hukumu ya kunyongwa haina mbadala'
Video: Liverpool yaacha kilio Stamford Bridge, Ni baada ya kuitungua Chelsea darajani