Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amezungumzia uhusiano wake na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na jinsi michango yake Bungeni ilivyokuwa inahusishwa na uhusiano huo.

Bashe ameeleza kuwa hoja zake zinazokosoa baadhi ya uamuzi na mipango ya Serikali haukuwa unatokana na kuondoka kwa Lowassa ndani ya chama hicho kama baadhi ya watu walivyokuwa wanadai, kutokana na jinsi alivyokuwa anamuunga mkono.

“Leo Lowassa yuko CCM, si aliondoka [kwenda Chadema] na sasa amerudi CCM! Jiulize, hivi Bashe amebadilika kuzungumza anachokiamini Bungeni?” Mwananchi inamkariri Bashe.

“Ninaunga mkono jambo ninaloamini ni sahihi, nitalisema na ndio utaratibu wangu,” aliongeza mbunge huyo na kuweka msimamo kuwa siku zote akiwa jukwaani ataipigania CCM lakini akiwa ndani ya Bunge atafanya wajibu wake kama mbunge wa kuwakilisha kile ambacho wananchi wamemtuma.

“Ninapozungumza bungeni ninatanguliza maslahi ya wananchhi wa Jimbo la Nzega, wananchi wa Tanzania na chama changu na mwisho wa siku maslahi ya Tanzania ni makubwa zaidi kuliko ya vyama vya siasa,” alisema.

Bashe aliyekuwa anamuunga mkono Lowassa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 2015, alieleza kuwa baada ya jina la mwanasiasa huyo kuondolewa kwenye mchakato yeye ndiye aliyemfuata nyumbani kwake na kumtaka afike kwenye mkutano mkuu.

Alisema ni utamaduni wa chama hicho kuwa kabla ya kumpata mgombea mmoja wa Urais, kila mwanachama ana haki ya kumuunga mkono mtu yeyote anayewania nafasi hiyo, lakini anapopatikana mgombea mmoja wote huungana na kumnadi.

Mwaka 2015, baada ya jina lake kuondolewa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Lowassa alijiunga na Chadema na kugombea nafasi hiyo akiungwa mkono na vyama vingine vilivyounga Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mwaka huu, mwanasiasa huyo alitangaza kurejea tena CCM akitoa sababu kwa ufupi, “nimerudi nyumbani.” Aliwataka watu milioni 6 waliompigia kura mwaka 2015 wamuunge mkono Rais John Magufuli.

Ethiopia: Mkuu wa majeshi auawa kwenye jaribio la Mapinduzi
Marekani yashambulia mifumo ya makombora ya Iran