Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ulinzi wa kutosha kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Asia Msangi ili kuondoa uzushi kuwa mgombea huyo anataka kutekwa.

Ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni za jimbo hilo uliofanyika Mziga Mwanagati, jijini Dar es Salaam, ambapo Bashe amesema kuwa kuna taarifa zimetolewa na watu wa Chadema wakidai wamepata taarifa kuwa mgombea wao atatekwa, hivyo ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama vikahakikisha vinamlinda.

Amesema kuwa si vyema kupuuza maneno hayo kwani wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni walipuuza yakatokea maafa.

“Nimesikia wakitoa hoja kuwa CCM wanataka kumteka mgombea wao, vyombo vya ulinzi naomba mtoe ulinzi kwa huyu dada alindwe kuanzia nyumbani kwake, kwenye gari na kwenye kampeni ili isije ikafika mahali wakaanza kusema ametekwa,” amesema Bashe.

Pamoja na mambo mengine, Bashe amesema chama chao kimejipanga hivyo ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakatenda haki.

Aidha, Bashe amewataka viongozi wa upinzani kuacha kusema kuwa wanaohamia CCM wamenunuliwa kwani kuna wengi wamehama chama tawala na kwenda upinzani lakini hakuna aliyesema amenunuliwa.

Hata hivyo, kwa upande wake Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, amesema tatizo la upinzani wakipelekewa ulinzi wanasema CCM imewapelekea mashushushu.

Video: Kucha, Kope bandia marufuku, Milioni 50 kila kijiji zasitishwa
55 kupigiwa kura Fifpro World XI