Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amekosoa mfumo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kupata viongozi wa chama hicho.

Bashe ambaye ni miongoni mwa wabunge wapya machachari wa CCM ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema kuwa kufanya uchaguzi kwa mtindo aliouita ‘gulio’ ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikikabili chama hicho katika chaguzi zake.

“Ni aibu CCM miaka hamsini, leo mfumo wa kupata viongozi ni gulio, matokeo yake chama kinagawanyika,” Bashe anakaririwa na Mwananchi.

“Uhuru wa kufikiri na kusema ukweli unaathirika kwa kuwa gulio linajenga matabaka na viongozi dhaifu ambao hawataki kusikia mawazo kinzani na tunajengeana hofu na taswira ya nidhamu ya uwoga,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, kada huyo wa CCM amesema kuwa udhaifu katika udhibiti wa rasilimali za chama hicho ni changamoto kubwa iliyokikumba chama hicho na kwamba anaamini chini ya Uenyekiti wa Dkt. John Magufuli (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), itadhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa kwakuwa Rais Magufuli hakutokana na kundi lolote lililokuwa linavutana ndani ya chama hicho, anayo nafasi kubwa ya kujenga misingi imara ya kusimamia haki.

“Kwakuwa Rais Magufuli hatokani na magenge yetu ya ndani, ana fursa nzuri sana kukifanya chama hiki kuwa imara kiuchumi bila kufukua makaburi,” alisema.

 

Claudio Ranieri Kumnoa Kivingine Riyad Mahrez
Ridhiwani Kikwete: Kuna Tatizo Yanga