Watu wanne wamefariki, na wengine 16 kujeruhiwa baada ya kuteketea kwa moto kufuatia kutokea kwa ajali ya basi dogo la abiria kuwaka moto kando ya barabara kuu ya Lagos-Ibadan nchini Nigeria.

Kikosi cha Usalama Barabarani cha Shirikisho (FRSC), kimesema katika ajali hiyo ya basi aina ya Mazda lenye namba za usajili APP934XH, kuliwepo na watu 20 na tukio hilo lilitokea majira ya saa 01:50 asubuhi kati aeneo lililo karibu na Oniworo, mbele ya kambi ya Foursquare, Jimbo la Ogun Nigeria.

Msemaji wa Ogun FRSC, Florence Okpe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema wanaume 15 na mwanamke mmoja walijeruhiwa, huku abiria wanne waliosalia wakiteketezwa kwa moto na hawakuweza kutambuliwa.

“Chanzo kinachoshukiwa kuwa kisababishi cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva uliosababisha kupoteza udhibiti na kupelekea basi kugonga ukingo wa kati wa barabara (kigawanyiko cha barabara) na kuwaka moto,” amefafanua Okpe.

Amesema, majeruhi waliopata majeraha wamepelekwa katika hospitali ya Victory iliyoko Ogere, huku Kamanda wa Sekta ya Ogun FRSC, Ahmed Umar akiwaonya madereva juu ya kuzingatia na kuepuka masuala ya mwendokasi huku akiwashauri kutii sheria na kanuni za trafiki.

Hata hivyo, Umar ametoa pole kwa familia za marehemu, huku akimuomba Mwenyezi Mungu kuzitia nguvu za kubeba hasara walizozipata na kuwapa faraja.

Amuuwa baba yake kwa kuoa mke wa pili
Watanzania watakiwa kuenzi uzalendo