Meneja kutoka nchini Ureno na klabu ya Man Utd, Jose Mourinho ameripotiwa kumtosa kiungo kutoka Ujerumani, Bastian Schweinsteiger katika kikosi chake ambacho kwa sasa kinajiandaa na msimu wa 2016/17.

Mourinho ameripotiwa kumtaka kiungo huyo kuanza kutafuta klabu ya kuitumikia kuanzia msimu ujao wa ligi, kutokana na kumuengua kwenye mipango yake ambayo ataanza kuitumia klabuni hapo mwezi ujao mara baada ya kuanza kwa mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini England.

Schweinsteiger, amefikishiwa ujumbe huo na Mourinho, sambamba na wachezaji wengine wanane ambao wameenguliwa kwenye kikosi cha mashetani hao wekundu wa Old Trafford kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Taarifa za kuondoka kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31, zilianza kuchukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari siku chache baada ya Mourinho kukabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo.

Sababu kubwa iliyokua inatajwa ni hali ya kiafya ya Schweinsteiger, ambayo kila msimu imekua na mgogoro kwa kupata majeraha ya mara kwa mara, hatua ambayo ilichangia kuachwa kwenye kikosi cha mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich mwishoni mwa msimu wa 2014/15.

Wengine walioarifiwa kutokua katika mipango ya Jose Mourinho ni wachezaji vijana Tim Fosu-Mensah, Cameron Borthwick-Jackson, James Wilson, Will Keane, Tyler Blackett na Paddy McNair.

Kutokuwepo kwa Andreas Perreira na Adnan Januzaj kwenye kikosi cha Man Utd ambacho kwa sasa kipo kambini kikijiandaa na msimu mpya wa ligi, napo kumezua hisia huenda wawili hao wakaachwa katika mipango Mourinho.

Pep Guardiola Asisitiza Usajili Wa Leroy Sane, John Stones.
MO: Nipo Tayari Kuwekeza Bilion 20 Msimbazi