Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kulitaka Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA) kusitisha mpango wao wa kukutana Dodoma kuzuia kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, Baraza hilo limetangaza mtindo mwingine wa kuingia mjini hapo.

Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrobas Katambi amesema kuwa Baraza hilo limepanga kufanya mkutano wake wa Kamati ya Utendaji kuanzia Julai 20 mwaka mjini Dodoma kwa lengo la kujadili muelekeo wa Demokrasia nchini.

“Kikao chetu cha Kamati ya Utendaji tulikuwa tumekiahirisha baada ya polisi kuzuia, lakini sasa tunafanya tena kwa tarehe ileile ambayo ni Julai 20 mjini Dodoma ambapo tulipanga kufanya mwanzo,” Patrobasi Katambi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Aidha, amewataka vijana wa chama hicho nchi nzima kuendelea kuwa watulivu na kutii agizo la Mwenyekiti wa chama hicho la kutoingilia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao utafanikisha kumkabidhi Rais John Magufuli Uenyekiti wa chama hicho, Julai 23.

Patrobas alilitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo wa CCM akisema kuwa inaonesha kushindwa kusimamia utekelezaji wa amri zake. Alidai kuwa Mkuu wa Jeshi hlo, IGP Ernest Mangu anapaswa kujiuzulu endapo ataruhusu kufanyika kwa mkutano huo.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi liliwakamata na kuwafikisha mahakamani viongozi wa BAVICHA waliokuwa mjini Dodoma akiwemo Mwenyekiti wake, kwa tuhuma za kutaka kuhamasisha vurugu na kuvaa fulana zenye maandishi yanayolenga kuikashfu Serikali. Viongozi hao wako nje kwa dhamana.

Mrema: Mbona haya hamumuulizi Rais mnanionea mimi?
Young Africans Yajichimbia Kaburi Kombe La Shirikisho