Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) limeendelea kutema cheche baada ya kupigwa marufuku na Jeshi la Polisi kukutana mjini Dodoma wiki hii wakati Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ukiwa mbioni kuanza.

Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi amesema kuwa Baraza hilo haliogopi hatua zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwakamata, kuwahoji na kuwafungulia mashtaka viongozi wake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ole Sosopi ambaye amesema kuwa Jeshi la Polisi limemtaka kufika tena kituoni tarehe 1 Agosti mwaka huu kwa ajili ya kumhoji baada ya kumhoji mara mbili hivi karibuni. Amesema kuwa jeshi hilo linapaswa kutofanya kazi kwa kufuata maagizo ya kisiasa bali lizangatie weledi.

“Nalitaka Jeshi la Polisi liache kufanya kazi kwa maagizo ya wanasiasa na badala yake lizingatie weledi. Lisijihusishe na propaganda za kisiasa, lifuate taaluma ili lisiendelee kupoteza heshima na mvuto mbele ya umma,” Sosopi aliuambia mtandao wa Mwanahalisi Online.

Amelitupia lawama Jeshi hilo kwa kumuita mara kwa mara kwa ajili ya kumhoji akidai linamsababisha kushindwa kufanya shughuli zake kwa ufanisi kama kiongozi wa chama lakini pia shughuli binasi zinazomuingizia kipato. Sosopi amelitaka Jeshi hilo kuchagua kumuacha huru au kumfikisha mahakamani.

Kiongozi huyo wa BAVICHA alikamatwa na Jeshi la Polisi mjini Iringa na kupelekwa jijini Dar es Salaam kuhojiwa baada ya kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi katika mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wafuasi wa Chadema, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Bavicha wamepanga kufanya mkutano wa ndani wa Kiutendaji jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuibuka na kile walichodai ni ‘mbinu mpya’.

Majaliwa Apokea Milioni 50 Kutoka NSSF, Ujenzi wa Shule Mpya Lindi
CCM yapeleka neema Dodoma, yashika hotel 306, Kinana ang’atuka