Siku chache baada ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kulionya Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) kuhusu mpango wao wa kwenda mjini Dodoma kwa lengo la kusaidiana na polisi kuzuia mkutano mkuu maalum wa CCM, vijana hao wa chama hicho kikuu cha upinzani wamejibu mapigo.

Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi ambaye jana alihojiwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za uchochezi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Baraza hilo halitanii na kwamba tayari limeshaandaa vijana 4,000 kwa kazi hiyo.

Alisema kuwa aliposikia kauli ya viongozi wa UVCCM alitegemea Jeshi la Polisi lingewachukulia hatua kutoa kauli za vitisho lakini imekuwa tofauti.

“Hatutanii hata kidogo na wala CCM wasidhani kuwa hatutakwenda Dodoma lakini tunaliomba Jeshi la Polisi litende haki juu ya kauli za uchochezi kwani nilitegemea viongozi wa UVCCM wangekamatwa na jeshi hilo lakini tunaokamatwa ni sisi tu, alisema Ole Sosopi.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamad Shaka alisema kuwa hawatawaruhusu BAVICHA kuingilia mkutano wao na kwamba watatumia kila mbinu kuwazuia na itakuwa kama ‘maumau’ ya Kenya.

Sosopi alisema kuwa baada ya Rais kupiga marufuku mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020, CCM walifurahi wakidhani kuwa wapinzani wamekomeshwa lakini sasa imekuwa zamu yao. Alihoji iweje Polisi wawazuie wapinzani na wawaruhusu CCM kufanya mikutano.

Sosopi alihojiwa jana na Jeshi la Polisi kutokana na kauli alizozitoa wakati wa sherehe za mahafali ya wanavyuo wanachama wa Chadema (CHASO) jijini Dar es Salaam, Juni 18 mwaka huu.

CCM imepanga kufanya Mkutano Mkuu Maalum utakaolenga katika kumkabidhi Uenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kutoka kwa mtangulizi wake, Dk. Jakaya Kikwete.

 

 

Video: Blue afunguka alivyosaidia ‘mtoko’ wa Diamond, uhusiano wa mapenzi na Wema, mafanikio, ujana…
Dk. Shein amtaka Maalim Seif kusahau ‘Serikali ya Mpito’, Seif adai yuko tayari kukamatwa