Sakata la rushwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano linaendelea kuumiza vichwa vya wadau wa maendeleo nchini huku taarifa zaidi zikizidi kutolewa kuhusu uwepo wa rushwa ndani ya Jumba hilo la wawakilishi wa wananchi kwa muda mrefu.

Taarifa zilizotolewa hivi karibuni na chanzo cha kuaminika zimeeleza kuwa wabunge waliokuwa anaunda Kamati mbalimbali walikuwa na bei zao elekezi na zilizokuwa zinajulikana kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya Taasisi na Mashirika ya Umma.

Chanzo cha ndani ya Bunge cha gazeti la Dira ya Mtanzania kimeeleza kuwa bei hizo za rushwa zilipangwa kulingana na Kamati husika za Bunge kutokana na umuhimu wake, na hii inaweza kuwa kati ya sababu ya baadhi ya wabunge kupigana vikumbe kuingia katika Kamati nyeti za Masuala ya Fedha.

Chanzo hicho kilieleza kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati hizo walikuwa wanapokea rushwa kama sehemu ya utaratibu wa mazoea kutokana namna walivyokuwa wanaona baadhi ya watendaji katika mihimili mingine wakipokea rushwa bila kuchukuliwa hatua stahiki.

Lakini pia, kilifafanua kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanyika katika Awamu zilizopita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi na ndio sababu hivi sasa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli imeibua kashfa nzito ambazo Bunge lilikuwa limezifumbia macho kutokana na kuwepo kwa baadhi wanaopokea ‘milungula’ minono.

“Ndio maana unaona Utawala wa Magufuli umeingia unakamata madudu ambayo hata Bungeni hayakupata kusikika utadhani bunge halikuwepo, kwa mwendo huu serikali italifunika Bunge,” Chanzo hicho kilieleza.

Aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), alieleza kuwa suala la rushwa kwa Wabunge sio tu kwa wabunge wa Kamati bali hata wakati wa Bajeti kuna baadhi hupokea rushwa ili kuitetea.

“Tulikuwa tuanaongea sana kuhusu suala hilo la rushwa na haipo katika kamati tu bali hata wakati wa Bajeti uwa zinaleta shida na usumbufu,” alisema Mkosamali huku akitoa mfano wa sakata la Tanesco wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini akiwa David Jairo, ambapo inaelezwa kuwa baadhi ya Wabunge walipokea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutetea.

'Nyoka' watumika Wizi wa Maji Dar
Vanessa Mdee azungumzia mpango wa kufunga ndoa