Klabu ya Borussia Dortmund imethibitisha kwamba Jude Bellingham atajiunga na Real Madrid baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili.

Madrid ilikubali italipa Pauni 115 milioni kwa ajili ya kiungo huyo wa kimataifa wa England na taarifa hiyo rasmi ikaandikwa kupitia tovuti ya Borussia Dortmund.

“Jude Bellingham anakaribia kujiunga na Real Madrid, tumefikia makubaliano pande zote, taratibu nyingine zitafuata mpaka uhamisho wake ukamilike. Aidha, itategemea na uwasilishaji wa nyaraka kwa wakati kwa mujibu wa masharti ya mfumo wa TMS.”

Borussia ikathibitisha kwa mara nyingine Madrid itatoa kwanza Pauni 88 milioni halafu baadae itamalizia Pauni 27 milioni.

Ada kama hizo za uhamisho zinategemea na mafanikio watakayopata Real Madrid au mchezaji katika kipindi cha miaka sita atakayocheza.

Kutokana na hayo, wasimamizi wanatarajia matokeo chanya ya takwimu muhimu za mapato ya mwaka wa fedha wa 2023/2024, Bellingham amekuwa gumzo Ulaya nzima kwa ubora wake.

Kiungo huyo ni chaguo namba moja la Meneja Carlo Ancelotti katika dirisha la usajili la kiangazi na hatimaye Borussia imekubali kumuuza.

Sasa Bellingham atapimwa afya siku chache zijazo kabla ya kutambulishwa rasmi kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, kwa mujibu wa ripoti.

Bellingham mwenye umri wa miaka 19, amefunga mabao 24 katika mechi 132 alizocheza Dortmund, vilevile akabeba DFB Pokal mwaka 2021. Amekuwa pia ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya England.

Wanajeshi wawili wafariki kwa ajali ya Helikopta
Serikali Wafanyabiashara wajadili ukuzaji wa masoko