Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo Septamba 28, 2021 amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika masuala mbalimbali ya kuinua uchumi hapa nchini.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amemuhakikishia Dkt. Ghanem kwamba serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika kuinua sekta binafsi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini kwa ushirikiano na wawekezaji.

Aidha Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema ili kukidhi mahitaji ya sekta binafsi hapa nchini serikali imeweka mkazo katika sekta ya elimu hasa elimu ya ufundi ili kupata wahitimu wenye ujuzi watakaoweza kusaidia kuinua sekta hiyo.

Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha utawala bora pamoja na kudhibiti rushwa hapa nchini hivyo kuweka mazingira rafiki ya kutekeleza miradi mbalimbali.

Kwa upande wake makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem amesema Benki ya Dunia itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali kama uboreshaji miundombinu ikiwemo ya Nishati na Tehama, mapambano dhidi ya uviko19 pamoja na kuinua uchumi baada ya janga la Uviko 19.

Taasisi ya JKCI kupima Moyo bure
Wakuu wa Mikoa wana jukumu kubwa mradi wa ECOP: Waziri Makamba