Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi 22 zilizoko Kanda ya Afrika, Anne Kabagambe amemhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kuwa Benki hiyo iko tayari kutoa kwa Tanzania fedha zote za mkopo wa masharti nafuu kiasi cha dola za marekani bilioni 1.7 zilizobaki katika mgao wa 18 wa IDA.

Kabagambe ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi amesema hayo wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, yaliyofanyika Jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutolewa kabla ya kuanza mgao mpya wa 19 wa IDA utakaoanza Julai 2020, baada ya kukamilisha taratibu zote za upatikanaji wa fedha hizo.

”Fedha hizi zitaelekezwa katika kutekeleza miradi kadhaa muhimu ikiwemo ya Elimu, Afya, Mradi wa kusaidia Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF, Awamu ya Pili na Uendelezaji wa Miji na Masuala ya Uchumi Jumuishi Visiwani Zanzibar,”amesema Kabagambe

Aidha, amepongeza hatua kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli, katika kupiga vita rushwa na ufisadi nchini pamoja na kutekeleza miradi ya jamii kwa umahili mkubwa ikiwemo miradi ya kimkakati ya reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa pamoja na mradi wa kufua umeme wa maporomoko ya maji katika mto Rufiji.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameiomba Benki hiyo kuisaidia Serikali kwa kuipatia fedha za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya umeme, reli, maji safi na salama, kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, bandari, rasilimali watu na masuala ya teknolojia ya habari na Mawasiliano-TEHAMA.

Amebainisha kuwa miradi hiyo itachochea zaidi ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa wananchi kwa kuwa nishati ya umeme itachochea ukuaji wa sekta ya viwanda hivyo na kukuza ajira, wakati reli imara na ya kisasa itaimarisha mtandao wa reli na kuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Afrika kwa ujumla.

Amepongeza pia uamuzi wa Benki hiyo wa kuruhusu upatikanaji wa fedha kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.7 na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi iliyokusudiwa katika sekta ya elimu, kusaidia kaya maskini kupitia TASAF, kuendeleza masuala ya uchumi jumuishi Visiwani Zanzibar, masuala ya ardhi na miundombinu ya barabara ili kuboresha shughuli za kiuchumi katika jamii.

Akitoa majumuisho ya mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na Mgeni wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamis Shaaban, amesema kuwa Serikali inapongeza uamuzi wa Benki wa kuendelea kuipatia fedha serikali ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi.

Mpaka sasa, Benki ya Dunia imefadhili miradi 28 ya Maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.0 sawa na takribani sh. trilioni 11.5, ambapo miradi 20 ni ya kitaifa yenye thamani ya dola 4.065 bilioni na miradi 8 ni ya kikanda yenye jumla ya dola za Marekani 938 milioni.

Video: Serikali yaunga mkono Mikopo kwa Wasusi, Kopa fasta, Bila dhamana
Bunge la Uganda lapinga hukumu ya kifo