Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed ameiasa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuwezesha wakulima ili waweze kuchangamkia fursa za kuuza mazao ya kilimo nje ya nchi ili kuwaongezea kipato wakulima hao.

Ameyasema hayo mapema hii leo alipotembelea alipolitembelea Banda la TADB katika Viwanja vya Ngongo mjini Lindi wakati wa Maonyesho ya Nane Nane yanayoendelea mkoani humo.

Amesema kuwa Tanzania inapata fursa nyingi za masoko nje ya nchi kwa mazao mbalimbali ikiwemo zao la karafuu, korosho na mazao ya mikunde ikiwemo dengu na mbaazi zinazotakiwa sana nchini India na Arabuni.

“Naiomba Benki ya Kilimo kuwawezesha wakulima wanaolima kibiashara ili kuchangamkia fursa za masoko kwa mazao ya kimkakati yakiwemo zao la karafuu, korosho na mazao ya mikunde ikiwemo dengu na mbaazi ambazo nchi nyingi marafiki wanahitaji,” amesema Hamad.

Aidha, ameongeza kuwa kuna wafanyabiashara wa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu wanaohitaji zaidi ya kontena mbili za korosho kwa wiki hivyo Benki ya Kilimo ina wajibu wa kuwezesha wakulima ili waweze kuchangamkia fursa hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis Assenga amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa TADB ni kuchagiza juhudi za Serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania.

Hata hivyo, ameongeza kuwa katika kutekeleza hayo Benki ya kilimo imedhamiria na kujizatiti katika kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

 

Video: Fahamu ustaarabu wa kustaajabisha Tanga na siri ya barabara 21
Picha za matukio mbalimbali katika Tamasha la Simba Day