Benki ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.46 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3.3 kwa ajili ya kujenga kipande cha Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Dodoma.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bill Winters.

Dkt. Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa kukubali kugharamia ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa ambayo lengo lake ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwenda bara na nchi jirani za Maziwa Makuu na zile ambazo hazipakani na Bahari.

“Tunajenga Reli hiyo ya Kisasa kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Makutupora ambazo ni awamu mbili lakini pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa nchi ya Rwanda, tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali” Amesema Dkt. Mpango

Hata hivyo, Dkt. Mpango amemweleza Kiongozi huyo wa Juu kabisa wa Benki ya Standard Chartered Group anayeongoza Benki hiyo kwenye nchi zaidi ya 60 duniani, kuhusu vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwemo kuboresha Shirika la Ndege la Taifa-ATCL, na Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji.

 

JKCI yasaini mkataba wa ushirikiano na Hospitali ya Moyo ya Fuwai
Real Madrid yawashiwa taa ya kijani usajili wa Mariano