Benki ya Standard Chartered Tanzania imezindua mfumo mpya wa matumizi ya teknolojia ya kidijitali ambayo inawezesha wateja wake kupata huduma zaidi ya 70 za kujihudumia wenyewe pamoja na huduma mbalimbali za kibenki kwa urahisi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mfumo huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani amesema kuwa mfumo huo utawawezesha wateja wa Benki ya Standard Chartered kujipatia huduma za kibenki kulingana na matakwa yao.

Amesema kuwa kupitia huduma hiyo, wateja wanaweza kufurahia ofa mbalimbali kama vile kutotozwa malipo katika kulipa ankara, malipo ya akaunti ya mwezi, kutokuwepo kwa kiwango cha akiba ya kufungua akaunti, matumizi ya mashine za kutoa fedha (ATM) au kadi za kutolea fedha na miamala ya kuhamisha fedha kwa njia ya mtandao kwenye akaunti za Standard Chartered.

Aidha, amesema mfumo huo umelenga kuwapatia wateja fursa ya kufurahia huduma za kibenki zaidi kupitia njia za kisasa zinazorahisiha maisha, mtu yeyote anaweza kujiunga na Benki kwa kupakua Programu hiyo kupitia simu yake ya mkononi.

”Kwa muda mrefu tumekuwa tukitoa huduma bora kwa wateja wetu, tunayo furaha kuzindua programu hii ya kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma za kibenki hapa nchini Tanzania. huu ni mwendelezo wa safari yetu muhimu ya matumizi ya teknolojia za kidijitali kama Benki na kudhihirisha dhamira yetu ya kuendelea kuwekeza katika kuleta mapinduzi ya kiteknolojia ya kisasa, kujenga mifumo na kuimarisha watu wetu tukiendelea kutumia mifumo yetu na ujuzi wa ngazi ya kimataifa kuleta mabadiliko ya uhakika ya matumizi ya teknolojia ya kidigitali nchini Tanzania.”amesema Rughani

Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za kibenki wa Standard Chartered, Ajmair Riaz amesema kuwa wateja wa zama za sasa wanahitaji kupata huduma bora na wanatafuta huduma na washirika ambao wanaweza kuwapatia huduma zinazopatikana kirahisi, kwa gharama nafuu.

Benki ya Standard Chartered inafanya kazi na msanii maarufu wa Tanzania, Vanessa Mdee ambaye atakuwa ni mwakilishi wa huduma hiyo kwenye promosheni mbalimbali.

Hata hivyo, Programu hiyo inaweza kupakuliwa au kuboreshwa kupitia Progamu za simu za kisasa za Google play store au Apple Store na baada ya zoezi hilo mtu anaweza kufungua akaunti ya Benki ya Standard Chartered kwa njia ya mtandao ndani ya muda usiozidi dakika 15.

Video: Fahamu tabia za wasichana wenye dimpoz
Wafanyabiashara Tarime wapokea mradi wa bil. 8

Comments

comments