Aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje wa Awamu ya Nne, Bernard Membe ametia mguu katika kesi ya mwandishi wa Habari za uchunguzi, Erick Kabendera kutaka aachiwe bila masharti yeyote.

Membe anakuwa kiongozi wa pili wa ngazi za juu kuungana na baadhi ya Watanzania wanaotaka Kabendera aachiwe huru baada ya mbunge wa Kigoma Mjini, ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kutoa kauli hiyo na kuanzisha kampeni mtandaoni kutaka mwandishi huyo aachiwe huru.

Membe amesema kuwa anaungana na mamia ya wananchi waliounga mkono kampeni ya Zitto ya kutaka Kabendera aachiwe huru bila masharti yoyote.

Aidha, katika ukurasa wake kijamii, Membe ameandika kuwa anaungana na mama mzazi wa Kabendera kupaza sauti kuomba serikali imuachie huru bila masharti yoyote mwandishi huyo wa habari za uchunguzi.

Amesema kuwa Tanzania ni nchi kubwa na ina sifa kubwa ya kutenda haki na uhuru wa kukumbatia uhuru wa waandishi wa habari.

”Niungane na mama mzazi wa Erick Kabendera na Watanzania wengi kupaza sauti yangu kuomba serikali imuachie Erick Kabendera bila masharti yoyote, Tanzania ina sifa moja kubwa nayo ni kutenda haki,”ameandika Membe katika ukurasa wake wa kijamii

Hata hivyo, ni mara chache sana kwa kiongozi aliyewahi kushika nafasi ya juu serikalini kutoa msimamo na mawazo yake hadharani na kutaka haki itendeke.

 

Ditopile awapa shavu UVCCM Dar
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 8, 2019