Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans Bernard Morrison amewaomba mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es salaam siku ya Jumapili, kushuhudia mpambano wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC).

Kiungo huyo mwenye ‘mbwembwe’ ametoa wito huo kwa mashabiki na wanachama, baada ya kuifungia bao la ushindi Young Africans kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar juzi Jumatano Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Young Africans Jumapili watapapatuana na Simba SC katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC), mchezo unaosubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki wa timu hizo mbili, zote za Dar es salaam.

Morrison, amesema goli alilolifunga dhidi ya Kagera Sugar linampa morari ya kufanya vizuri kwenye mchezo unaofuata, na kuisaidia timu yake kutinga hatua ya Fainali Kombe La Shirikisho.

Amesema mashabiki hawana haja ya kuwa na hofu na mchezo huo kwa kuwa yeye na wachezaji wenzake wanatambua umuhimu wa mchezo huo.

“Lengo ni kufanya vyema na kuhakikisha tunacheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, tunafahamu ndio tiketi yetu ya pekee kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao,” amesema Morrison

“Muda uliobakia naamini benchi la ufundi litaendelea kutuandaa na kutujenga kwa mchezo huo, tusubiri siku ifike,” ameongeza kiungo huyo kutoka Ghana.

Morrison ni kama ameamsha hisia za mashabiki wa Young Africans kuelekea kwenye mchezo huo wa Jumapili kutokana na bao alilofunga dhidi ya Kagera.

Kabla ya mchezo huo kulikuwa na sintofahamu kwa mashabiki kujua mustakabali wa kiungo huyo kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Simba SC.

Ni wazi sasa uwepo wake kwenye mchezo huo utawapa shauku kubwa mashabiki wa Young Africans kuelekea kwenye mchezo huo wa Jumapili.

Mshindi wa mchezo huo atatinga hatua ya fainali na kuchuana na mshindi baina ya Sahare ya Tanga na Namungo ya Lindi watakaocheza nusu fainali nyingine kesho Jumamosi.

FA waomba radhi kuchemsha kwa VAR
Mwinyi ndiye mgombea Urais 2020 Zanzibar