Wakati tetesi zikiendelea huenda akarudi Young Africans kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, Uongozi wa klabu ya Simba umetoa taarifa za kumpa mapumziko Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison hadi mwishoni mwa msimu huu.

Simba SC imetoa taarifa hiyo na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii leo Ijumaa (Mei 13), hali ambayo huenda ikaongeza uhakika wa kiungo huyo kuondoka mwishoni mwa msimu kufuatia mkataba wake kutarajia kufikia kikomo.
Taarifa za Simba imeeleza sababu za kufanya hivyo, ni kutaka kumpa muda wa kupumzika kiungo huyo hadi mwishoni mwa msimu huu, ili kutatua matatizo yake binafsi.

“Simba SC imefikia maamuzi haya baada ya pande zote mbili kukubaliana kwa lengo la kumpa nafasi Morrison kupumzika na kushughulikia mambo yake binfasi.”

“Tunatambua na kuthamini mchango wa Morrison katika miaka miwili aliyoitumikia klabu yetu na kuisaidia kupata mafanikio kadhaa ikiwemo kucheza Robo Fainali ya michuano ya Afrika Mara Mbili, Kuchukua Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports na Ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.” imeeleza sehemu ya barua ya klabu ya Simba SC.

Simba SC ipo katika mchakato wa kusaini mikataba mipya na baadhi ya wachezaji wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, lakini suala la Morrions limekua kizungumkuti kutokana na madai ya nidhamu yake ambayo haiwafurahishi baadhi ya viongozi klabuni hapo.

Baadhi ya Wachezaji wa Kimataifa wanaomaliza mikataba yao Simba SC ni Beki kutoka nchini Kenya Joash Onyango, Pascal Wawa (Ivory Coast), kiungo kutoka Zambia Rally Bwalya, Bernard Morrison (Ghana) na Mshambuliaji Criss Mugalu (DR Congo).

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) afariki dunia
Mnyika: Tumefikisha barua kwa Spika