Dunia ya mtandaoni imetikiswa leo, baada ya Beyonce Knowles kuachia ghafla mizigo miwili mizito, ambayo ni albam ya video inayoonesha alivyotumbuiza mubashara kwenye Tamasha la Coachella Valley Music and Arts mwaka 2018.

Albam hiyo na makala ambayo imeachiwa kupitia Netflix, zote zimepewa jina la ‘Homecoming’ na zinaonesha matukio ya kihistoria ya Beyonce. Kwanza ni namna alivyokuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike mweusi kuongoza tamasha la Coachella (headline). Beyonce alitumia wachezaji 100 jukwaani na walichokifanya hakijawahi kufanyika awali.

Kupitia makala yake, Beyonce anawaonesha mashabiki wake kilichofanyika nyuma ya pazia ya tamasha hilo kuanzia mpangilio mzima wa mazoezi hadi wageni walioalikwa kumsindikiza akiwemo mumewe Jay Z, dada yake Solange Knowles na wanafamilia wenzake wa Destiny’s Child, Kelly Rowland na Michelle Williams.

Baada ya tamasha hilo, Beyonce alitangaza kuwa ana mpango wa kutoa $100,000 kwa ajili ya kusaidia shule za kihistoria za watu weusi, kwa kuwasomesha wanafunzi (scholarship).

Awali, alikuwa amepangiwa kutumbuiza kwenye tamasha la mwaka 2017 lakini ilibidi achelewe baada ya kupata watoto wake mapacha, Sir na Rumi.

“Nilikuwa nacheza na kuimba jukwaani halafu natoka kidogo naenda kuwanyonyesha watoto, katika siku ambazo nilikuwa naweza nilikuwa nawapeleka watoto pia,” Beyonce anafunguka kwenye makala ya ‘Homecoming’.

Ingawa Netflix walikuwa wameshatangaza ujio wa makala hiyo kwa wiki kadhaa, mashabiki hawakuwa wanatarajia kupewa albam yenye nyimbo 40 nzito, zikiwa na nyimbo nyingine bora za muda wote kama “Crazy In Love,” “Say My Name” na “Single Ladies.” Kuna ngoma nyingi mpya pia ndani kama ‘Lift Every Voice and Sing’ ambao hutajwa kuwa ni wimbo wa Taifa wa watu weusi.

Mtandaoni, wadau wa muziki wameiweka ‘Homecoming’ kuwa kwenye kilele cha mijadala yake leo. Kwa mujibu wa takwimu za Netflix asilimia 97 wame-like makala hiyo ya video.

Mwanafunzi afariki dunia akipiga picha na wenzake
Familia ya Nipsey Hussle yakataa michango ya fedha kwa watoto

Comments

comments