Wawakilishi wa Tanzania kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika CAF, Klabu ya Biashara United Mara FC wamedhamiria kuwasilisha ofa ya kumsajili beki wa kati wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ibrahim Ame.

Dhamira kubwa ya kujipanga kuwasilisha ofa hiyo huko Msimbazi, imetokana na klabu hiyo kuachana na beki Abdul-Majid Mangalo baada ya kumaliza mkataba wake klabuni hapo .

Uongozi wa klabu hiyo ya mkoani Mara, unaamini endapo utafanikiwa kumnasa Ame, watakua na safu bora ya ulinzi hasa kwenye michuano ya kimataifa, kufuatia beki huyo wa zamani wa Coastal Union kujifunza mambo mengi wakati wa ushiriki wa Simba SC katika michuano ya kimataifa.

Mbali na Ame, Uongozi wa Biashara United umedhamiria kufanya usajili wa wachezaji wengine wenye uzoefu wa kimataifa, ili kuwa na kikosi bora na imara kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2021/22.

Kufuatia Tanzania kupata fursa ya kuwakilisha na klabu nne msimu ujao, Biashara United Mara FC iliyomaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu msimu wa 2020/21, inaungana na Azam FC ambayo pia itashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika CAF.

Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC na Young Africans iliyomaliza nafasi ya pili msimu wa 2020/21, watashiriki Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barania Afrika msimu ujao 2021/22.

Ripoti uchunguzi vifo vya samaki ufukweni
Masau Bwire amuaga Manara kwa ujumbe mzito