Biashara United Mara imejizatiti kuwakabili vilivyo Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, katika mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa keshokutwa Alhamis (Februari 18).

Simba SC ambayo jana Jumatatu (Februari 15) ilianza mandalizi jijini Dar es salaam, baada ya mapumziko ya siku moja, itasafiri hadi mjini Musoma, Mara kwa ajili ya mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.

Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuanza vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuifunga AS Vita Club ya DR Congo, bao 1-0 mwishoni mwa juma lililopita.

Hata hivyo Kocha Mkuu wa Biashara United Francis Baraza amesema anaendelea kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya mchezo huo na ana matarajio makubwa ya kubakisha alama tatu muhimu nyumbani.

Kocha huyo ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Januari 2021, amesema wanahitaji alama tatu za mchezo huo.

Amesema anakumbuka katika mzunguuko wa kwanza Simba SC iliwafunga mabao 4-0 jijini Dar es salam na kufanikiwa kuvuna alama zote tatu wakiwa nyumbani kwao, hivyo na upande wa Biashara United Mara wanahitaji kufanya hivyo wakiwa nyumbani Musoma, Mara.

“Ninawaamini wachezaji wangu na tayari maandalizi yameanza kwa ajili ya mchezo wetu muhimu ambao utakuwa na ushindani mkubwa.”

“Ninawatambua wapinzani wetu Simba namna ambavyo wanacheza pamoja na ubora wao, hatutawabeza tutawaheshimu, ina wachezaji wazuri ila wajue kwamba hata sisi tuna wachezaji wazuri.” Amesema kocha huyo raia wa Kenya.

Kwenye mchezo wao wa mwisho ndani ya Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili Biashara United Mara ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC, hivyo itaingia ndani ya uwanja kwa kujiamini.

Biashara United mara ipo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 32, huku Mabingwa watetezi Simba SC wakiwa nafasi ya pili wakiwa na alama 39.

Afrika yapata uongozi WTO
Tshisekedi ateua Waziri Mkuu mpya