Uongozi wa klabu ya Biashara United Mara umetangaza timu yao itautumia Uwanja wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza, kwa ajili ya michezo ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika CAF.

Biashara United Mara ambayo itashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa msimu huu 2021/22, imepangwa kucheza dhidi ya FC Dikhil ya Djibouti, mchezo wa hatua ya awali mwezi Septemba.

Mwenyekiti wa klabu ya hiyo yenye maskani yake makuu mjini Musoma mkoani Mara, Seleman Mataso amesema tayari wameshawasilisha barua TFF, huku wakipata baraka zote kutoka kwa wasimamizi wa Uwanja wa CCM Kirumba.

“Tumeshawasilisha barua yetu TFF ambayo imeeleza dhamira ya kuutumia Uwanja wa CCM Kirumba kwenye michuano ya kimataifa, nina imani TFF na CAF watatupa baraka zote za kuutumia Uwanja huu;”

“Uwanja wa CCM Kirumba upo karibu na hapa nyumbani Musoma, itakua rahisi kwetu kufanikisha mipango ya kwenda Mwanza na kurudi, ndio maana tumeona Uwanja wa CCM Kirumba ni mahala salama kwetu.”

“Tumewasiliana na wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba, wameonesha kufurahia sana maamuzi tulioyachukua ya kutumia Uwanja wao kwenye michuano ya kimataifa, hivyo wametupa baraka zote.” amesema Mataso.

Mchezo wa mkondo wa kwanza kati ya Biashara United Mara dhidi ya FC Dikhil ya Djibouti utapigwa kati ya Septemba 10 na 12, huku mchezo wa mkondo wa pili ukipangwa kuchezwa kati ya Septemba 17-19, mwaka huu.

Taliban wamewasihi watu kuondaka uwanja wa ndege
Gor Mahia kumsajili Francis Kahata