Mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguuko wa tatu kati ya Biashara United Mara dhidi ya Tanzania Prisons, uliokua umepangwa kuchezwa kesho Jumanne (Oktoba 19), umesogezwa mbele.

Mchezo huo uliotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, umesogezwa mbele ili kutoa nafasi kwa Biashara United Mara, kujiandaa na safari ya kuelekea mjini Tripoli, Libya tayari kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho mkondo wa pili, utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.

Meneja wa Biashara United Mara Frank Wabare amethibitisha taarifa za kuahirishwa kwa mchezo huo, huku akishukuru mamlaka ya soka nchini, kwa kufanya maamuzi ya busara ambayo yanawapa nafasi ya kujiandaa vizuri na safari ya kuelekea Libya, kwa mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Al Ahly Tripoli.

”Tunashukuru kwa mchezo huo kusogezwa mbele sasa tutapata muda wa kujifua kwa ajili ya mechezo wetu dhidi ya Al Ahly Tripoli ugenini, pia tutapa muda wa kushugulikia taratibu zote za safari kwa usahihi,”

“Kambi inaendelea hapa Dar na kila kitu kipo vizuri, tumepanga kusafiri Jumatano au Alhamisi kwa ndege ya kuunga kwani hakuna usafiri wa moja kwa moja hadi Libya, imani ya timu nzima ni kulinda ushindi wetu na kusonga mbele kwa hatua inayofuata ya michuano hiyo ya CAF.” amesema Frank Wabare

Naye Kocha mkuu wa Biashara Patrick Odhiambo Okumu amesema hatua ya kusogezwa mbele kwa mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi Tanzania Prisons, imempa wasaa mzuri wa kuendelea na program yake ya maandalizi ya kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili.

“Kuahirishwa kwa mchezo huo ni taarifa nzuri na imetufanya tuendelee kujinoa kwa ajili ya mechi ya Tripoli. Nimewaona wakicheza kwao, ni timu ngumu hivyo licha ya kwamba tuliifunga nyumbani, tutaenda kucheza kwa tahadhari kubwa ili tuweze kufuzu hatua inayofuata.” amesema Odhiambo

Biashara United Mara ipo mbele kwa mabao 2-0, waliyoyapata kwenye mchezo wa Mkondo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Ijumaa (Oktoba 15).

UVIKO 19 chanzo cha Ukosefu wa Ajira na Wimbi la Umasikini
Kocha Gomes afichua siri ya kushinda ugenini