Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameihakikishia Taasisi ya Sekta Binafsi TPSF ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini kwa kuwa Serikali inaamini uwepo wa sekta binafsi imara ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi imara wa Nchi.

Aidha Balozi Mulamula ameitaka TPSF kuhakikisha kuwa inakuwa na kanzi data ili kurahisisha azma ya Serikali ya kuiunganisha sekta hiyo na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutoka katika mataifa mengine ulimwenguni.

Hata hivyo TPSF imekiri uwepo wa ongezeko la biashara kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ushoroba wa kusini zikiwemo nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Angelina Ngalula amesema kuwa ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zikiwemo Kenya, Burundi na Uganda umeongezeka na kwamba ushirikiano kati ya Tanzania na Mataifa hayo umezidi kuimarika ukiashiria kukua kwa diplomasia ya uchumi.

Ameongeza kuwa ushirikiano ambao Serikali imekuwa ikiutoa kwa sekta binafsi umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na ushoroba wa kusini ikihusisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Waziri Mkuu ashukiwa mauaji ya Rais
Mkurugenzi Kishapu apewa siku saba zahanati ikamilike