Mshambuliaji wa Namungo FC Bigirimana Blaise, amekiri kufatwa na viongozi wa Young Africans, ili afanikishe lengo la kujiunga na klabu hiyo kwa msimu ujao wa ligi.

Bigirimana ambaye alijiunga na Namungo FC mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Alliance FC ya jijini Mwanza, amesaliwa na miezi michache, mkataba wake na Namungo FC ufikie kikomo.

Amesema baada ya kufuatwa na viongozi klabu hiyo kongwe nchini, aliwapa maelekezo ya kuwasiliana na meneja wake.

Hata hivyo mshambuliaji huyo kutoka nchini Burundi amesema bado ana mkataba na klabu ya Namungo FC na anauheshimu, hivyo hatofanya mipango yoyote ya njia za panya.

Amesema lengo lake ni kucheza soka kwa uhalali pasina matatizo na yoyote, hivyo atahakikisha taratibu zinafuatwa kama kweli viongozi wa Young Africans wanahitaji huduma yake.

“Ni kweli Yanga walikuja na nikawapa maelekezo ya kuonana na meneja wangu, hivyo wao ndio wanazungumza, kwa sasa naheshimu muda wa mkataba wangu uliobaki na Namungo.”

Mkataba wa Bigirimana na Namungo FC unatarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, na tayari mazungumzo kati yake na viongozi wa klabu hiyo ya mkoani Lindi yalishaanza.

“Namungo FC tulianza mazungumzo ila bado hatujafikia muafaka kutokana na hili janga la Corona, ila nina imani hivi karibuni tutarejea kukamilisha ligi na kuendelea kuzungumza na viongozi,” alisema Bigirimana.

Nchimbi: Kipigo cha Kagera Sugar kiliniuma
Magufuli ayamaliza na Kenyatta "Haiwezekeni kila dereva ana Corona"