Mshambuliaji wa klabu ya Namungo FC raia wa Burundi Bigirimana Blaise, ambaye amekuwa na kiwango bora katika msimu huu wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara, amesema meneja wake wamepokea ofa kutoka Afrika Kusini.

Awali Bigirimana ambaye msimu huu ametoa mchango mkubwa wa ushindi kwenye klabu ya Namungo FC, alihusishwa kujiunga na Young Africans akiwa mwishoni mwa mkataba wake, lakini pia timu kutoka Africa Kusini imeona uwezo wake na kuhitaji kumsajili nyota huyo.

Tumepata nafasi ya kuzungumza na nyota huyo akiweka wazi juu ya uhamisho huo kuwa, kama mambo yatakuwa safi atafanya maamuzi na kujiunga na moja ya klab itakayokua na ofa nzuri kwake.

“Taarifa za mimi kuhusishwa kujiunga na Young Africans ni kweli, Yanga walifika mezani kuzungumza na mimi wakihitaji niwe moja ya familia katika klabu hiyo msimu ujao, mtu ambaye anasimamia suala hilo ni meneja wangu.”

“Kuhusu Africa Kusini ndio meneja aliniambia hilo, kuwa kuna klabu moja ya ligi ya huko imeonesha kuhitaji huduma yangu kwa sasa kila kitu kipo chini ya meneja siwezi kusema sasa hivi kuwa msimu ujao nitakuwa wapi maana ofa zipo nyingi, yule ambaye ataweka ofa nzuri basi nitajiunga naye.” Alisema Bigirimana Blaise.

Hata hivyo uongozi wa Namungo FC bado unadaiwa kuwa kwenye mazungumzo na mshambuliaji huyo, kufuatia mkataba wake kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Waziri Jafo alitaka shirika la elimu Kibaha kuongeza ubinifu
Maofisa wawili TRA watiwa mbaroni kwa kuomba rushwa

Comments

comments