Kiungo kutoka nchini Burundi Gael Bigirimana amethibitisha kuondoka kwa salama na amani Young Africans, baada ya kuvunjwa kwa mkataba wake.

Kiungo huyo ambaye aliwahi kuitumikia Newcastle United inayoshiriki Ligi Kuu ya England kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, alisajiliwa Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akiwa mchezaji huru.

Bigirimana amesema aliondoka Dar es salaam Juzi Jumatatu (Januari 23) kurudi nchini kwao Burundi, ambako anajiandaa kuanza maisha mapya nje ya Klabu ya Young Africans.

“Nimerejea nyumbani Burundi tayari kwa kuanza maisha mengine mapya nje ya Young Africans baada ya kudumu kwa muda mfupi”

“Nimeondoka Young Africans baada ya kufikia muafaka mzuri na viongozi ambao tumekubaliana kuvunja mkataba wa mwaka mmoja na nusu uliokuwepo baina yetu.”

“Ninaamini ipo siku nitarudi tena Tanzania kucheza soka, nimejifunza vitu vingi kwa muda mfupi na nimeyapenda sana maisha ya hapo.” amesema Bigirimana

Katika hatua nyingine Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, ameitakia kila la kheri Young Africans katika mapambano yake ya kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara pamoja na ushiriki mzuri wa Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 56, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 50, huku Azam FC na Singida Big Stars zikibanana nafasi ya tatu na nne kwa kuwa na alama 43 kila mmoja.

Zaidi ya watu 1,000 wafariki kwa Kipindupindu
Serikali haitaki kusikia Wananchi wakilalamikia umeme: Makamba