Meneja wa klabu ya West Ham Utd Slaven Bilic, anaamini mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa alipaswa kuonyeshwa kadi nyekundu wakati wamchezo wa ligi ya nchini England ambao ulishuhudia wagonga nyundo wakikubali kufungwa mabao mawili kwa moja katika uwanja wa Stamford Bridge.

Bilic alisisitiza jambo hilo alipozungumza na kituo cha Sky Sports mara baada ya mchezo huo wa ufunguzi wa ligi kwa klabu hizo mbili.

Bilic alisema Costa alikua ameshaonyeshwa kadi ya njano kabla ya kufanya tukio la kumchezea hovyo mlinda mlango wa West Ham Utd Adrian, hivyo muamuzi Anthony Taylor alipaswa kumuadhibu kwa kumuonyesha kadi ya pili ya njano ambayo ingeambatana na nyekundu, lakini cha kushangaza aliashiria mpira wa adhabu kupigwa kuelekea upande wa The blues.

Diego Costa akimchezea rafu ya makusudi mlinda mlango wa West Ham Utd Adrian.

“Tayari alikua ameshaonyeshwa kadi ya njano,” Alisema Bilic

“Ilinishangaza kuona muamuzi anashindwa kufanya maamuzi sahihi, kwa sababu kitendo kilichofanywa na Costa kilikua hakihusiani na mpira.

“Lakini suala hilo halitotuvuruga na hatuna budi kuliacha kama lilivyo, tunakubali tumepoteza mchezo na tunajipanga na mpambano mwingine wa mwishoni mwa juma hili.”

Katika mchezo huo Chelsea walipata bao la kwanza kupitia kwa Eden Hazard kwa njia ya penati katika dakika ya 47 kabla ya James Collins kusawazisha katika dakika ya 77, lakini mshambuliaji kutoka nchini Hispania Diego Costa alifunga bao la ushindi kwa The Blues katika dakika ya 89.

Mvutano Wa Ada Ya Usajili Wavuruga Mipango Ya Inter Milan
Eneo la Ikulu lauzwa kinyamela