Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4. 6 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu katika wilaya hiyo, ambapo amesema kuwa lengo la kutekeleza mradi huo ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.

Amesema kuwa serikali imeweka mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya, kwani ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana wenye maarifa na stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.

“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” amesema Ole Nasha.

Wakati huo huo, Naibu Waziri ametoa miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanamaliza ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema hajaridhishwa na sababu zilizotolewa na mhandisi msanifu kutoka TBA zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Godwin Kitonka amesema kuwa Halmashauri yake inaishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ambayo ni pamoja na jengo la utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni la wasichana na kukarabati karakana ya ushonaji na uchomeleaji chuma.

 

Msemaji wa Serikali atoa neno kufuatia ajali ya lori la mafuta
Video: Alikiba, Ommy Dimpoz, Willy Paul waunganisha nguvu na kuachia 'Nishikilie'