Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan, jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa miji 28 wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha Waziri Aweso amemuomba Balozi Pradhan kuwezesha utekelezaji mzuri wa mradi mkubwa na muhimu wa kihistoria utakaoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Maji Tanzania, unaotarajiwa kuanza punde uweze kukamilika haraka iwezekanavyo na ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa.

Hata hivyo ameishukuru Serikali ya India kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi wa maji wa Igunga, Nzega na Tabora kwa kutoa fedha za mkopo wa masharti nafuu kupitia Exim Bank ya India pamoja na wakandarasi kutoka India waliofanya kazi nzuri na kuwezesha mradi kukamilika kwa wakati na kiwango bora.

Pia, Sambamba na hayo ameiomba India kuendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwenye Sekta ya Maji katika maeneo mbalimbali kwa dhumuni la kuinua kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama nchini.

Kwa upande wake Balozi Binaya Srikanta Pradhan, amemuhakikishia Waziri Aweso ushirikiano mkubwa kutoka Serikali ya India kwenye maeneo mbalimbali ya kisekta pamoja na kuwajengea uwezo wataalam kwenye maeneo kukabiliana na upotevu wa maji, usimamizi na uendeshaji wa miradi na ujenzi wa miradi.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan (kulia)katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Maji, Mtumba, jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa pamoja na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) katika kikao na Balozi wa India nchini kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Maji, Mtumba, jijini Dodoma.

Katibu Wizara ya Afya afanya mazungumzo na Mkurugenzi Benki ya Maendeleo Ujerumani
Miundombinu ya TANESCO kutumika Mkongo wa Taifa