Waziri wa Madini Doto Biteko, ametoa siku 60 za kufuta leseni za uchimbaji wa madini zilizohodhiwa na wawekezaji kwa muda mrefu bila kuzitumia, huku akibainisha kuwa Serikali imedhamiria kuinua Sekta ya Madini, pamoja na kumaliza migogoro yote ambayo hujitokeza baina ya wachimbaji wadogo na wakubwa.

Waziri Biteko ameyasema hayo wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga  Agosti 1, katika uwanja wa Zainab Teleck kijiji cha Butulwa kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga.

“Naomba mfikishe salamu kwa wawekezaji wa madini ambao wana leseni za uchimbaji na hawazitumii, tumetoa siku 60 tu zianze kutumika, zaidi ya hapo tutazitaifisha na kutoza gharama ambazo Serikali imeingia kutokana kutolipiwa kodi kwa muda mrefu na kusababisha Serikali kukosa mapato na fedha hizi lazima zilipwe hatutakuwa na msalia mtume, hatutaki migogoro ya uchimbaji wa madini,’’ Amesema Biteko.

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa katika banda la kampuni ya Barrick kwenye Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yaliyoanza Julai 23 katika uwanja wa Zainab Telack Kijiji cha Butulwa Manispaa ya Shinyanga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula ameunga mkono  kauli ya Waziri Biteko kwa kutoa siku 60 kwa wawekezaji ambao wanamiliki leseni za uchimbaji madini na kutoziendeleza kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria, pamoja na kufidia fedha ambazo zilipaswa kulipwa kwa kipindi chote walichohodhi leseni hizo.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) Hamza Tandiko amezishukuru Taasisi za kifedha kwa kuanza kuwapatia mikopo wachimbaji wa madini huku akiomba Serikali kupeleka umeme wenye nguvu ya kuendesha mitambo kwenye maeneo ya machimbo kwani umeme uliopo sasa ni kwa ajili ya mwanga tu.

Kabwili aomba radhi, akiri kufanya kosa
Rais Samia afanya uteuzi