Mvutano baina ya Balozi wa Uganda nchini Marekani, Mull Sebujja Katende na Mbunge Robert Kyagulanyi Ssentamu ulijitokeza Jumatano, wakati wa mahojiano na VOA -(Voice Of America) katika kipindi cha Straight Talk Africa kilichofanyika jijini Washington Marekani ambapo mbunge alimhoji balozi huyo ni kwa nini serikali ya Uganda inawatesa wananchi wake.

Wakati wa mahojiano hayo Mbunge Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine katika madai yake ameituhumu serikali ya Uganda kwa kuwatesa wananchi akionyesha yeye jinsi alivyoteswa baada ya kukamatwa na kikosi maalum cha kumlinda Rais Museveni, huku kwa upande wake Balozi Katende akisisitiza kuwa Uganda ni nchi inayo heshimu mfumo wa demokrasia, sheria na haki za kibinadamu.

Bobi Wine yupo nchini Marekani kwa matibabu baada ya kupata majeraha akiwa mikononi mwa kikosi maalum cha jeshi kufuatia kukamatwa kwake huko Arua mwezi Agosti, 2018 na kuteswa.

Aidha, kwa upande wake balozi amesema kuwa Uganda haiungi mkono mateso, ambapo amesema kuwa chochote kilichomtokea Bobi Wine wakati alipokamatwa na vyombo vya usalama nchini Uganda vinafanyiwa uchunguzi juu ya madai yake ya mateso aliyopata, hivyo amemtaka asubiri matokeo ya uchunguzi huo mpaka yatakapo fikishwa Mahakamani.

Hata hivyo, Balozi Katende amesema kuwa kinacho endelea Uganda kwa wapinzani ambao wana maoni tofauti, ambao wameshindwa kuwashawishi wananchi kuwapa kura kuingia katika bunge, wanaishia kufikiria kuwa njia mbadala iliyo bora ni kusababisha fujo na wapate ushindi kupitia machafuko ya kisiasa.

Benki Kuu yashusha rungu kwa mabenki yaliyotunza fedha za wizi
Kubenea awavuruga Chadema