Nahodha na Mshambuliaji wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Wekundu Wa Msimbazi Simba, John Bocco, amesema wataendelea kupambana kwenye michezo ya Ligi Kuu, ili kutimiza azma yao ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo.

Bocco alitoa kauli hiyo baada ya mchezo dhidi ya KMC FC usiku wa kuamkia leo, uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere, kwa njia ya mkwaju wa Penati.

Mshambuliaji huyo mzoefu katika soka la Bongo alisema wanafahamu ushindani umeongezeka zaidi na hali hiyo inawaongezea hamasa ya kujituma kwa sababu wapinzani wao pia wanayataka mafanikio.

“Kila siku tunaimarika, tunajiimarisha kwa ajili ya kusaka matokeo mazuri, kila timu inahitaji ubingwa, lakini sisi tunauhitaji zaidi kwa sababu uko mikononi mwetu,” Bocco alisema.

Aliongeza mbali na Ligi Kuu Tanzania Bara, mazoezi na maandalizi wanayofanya kila siku yanazingatia jukumu la kupeperusha bendera ya nchi ambalo wanalo.

Nyota huyo anayeongoza katika kupachika mabao alisema kwake anajipanga kujituma na kucheza katika kiwango bora kila atakapopata nafasi na anaamini kwa kufanya hivyo ataiweka timu yake kwenye nafasi nzuri.

Simba sasa inajiandaa na safari ya kuelekea nchini Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum itakayochezwa kati ya Desemba 22 na 23, mwaka huu jijini, Harare nchini humo.

Wawakilishi hao wa Tanzania Bara katika michuano hiyo ya kimataifa wakirejea nchini wataendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwakabili Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu utakaofanyika Desemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, Dar es Salaam na Desemba 30, mwaka huu watapambana dhidi ya Dodoma Jiji FC kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ushindi dhidi ya KMC FC umeendelea kuiweka Simba SC kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, huku ikifikisha alama 32, wakitanguliwa na Young Africans wenye alama 37, na Azam FC wapo nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 28.

Kortini kwa kosa la kutumia youtube bila kibali
Mahakama yaamuru Bilioni 5.4 za Mr. Kuku zitaifishwe