Waendesha Bodaboda 3,500 katika Kaunti ya Murang’a nchini Kenya, kwa kushirikiana na Shirika la Ahadi Kenya Trust wameazimia kuwasafirisha wagonjwa, wazee, watu wenye ulemavu na kina mama wajawazito katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, ili washiriki zoezi la kupiga kura.

Mkurugenzi wa Shirika hilo lisilo la Kiserikali la Ahadi Kenya Trust, Dkt. Stanley Kamau amesema kitendo hichp kinapaswa kupongezwa na kudai kuwa wanapanga kuwawezesha madereva hao kwa kutambua na kuwasaidia watu walio na changamoto zinazoweza kusababisha washindwe kushiriki upigaji wa kura.

Amesema Shirika lake limekusanya waendesha bodaboda wa kutosha katika kila wadi 35, ili kusaidia wazee na watu wenye ulemavu kufikia maeneo ambayo wanatakiwa kutimiza azma yao ya kikatiba ya kupiga kura Jumanne ya Agosti 9, 2022.

Waendesha Bodaboda nchini Kenya, (picha na KNA)

“Uchaguzi ni zoezi muhimu la kitaifa na baadhi ya wakazi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali wanahitaji kuungwa mkono ili kupiga kura zao, sasa kitendo cha bodaboda hawa kuonesha nia yao ya kuwsafirisha watu wenye uhitaji ni cha kupongezwa na tutawawezesha,” amesema Kamau.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Mwenyekiti wa waendesha bodaboda wa Mathioya, William Mwangi amesema kusafirisha wazee na watu wenye ulemavu hadi kituo cha kupigia kura ni njia mojawapo ya kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Amesema, “Tunashukuru kwa kitendo cha dhati cha Ahadi Kenya Trust kuwezesha kufanikisha azma yetu ya kuhakikisha wapiga kura wanajitokeza kwa wingi, wakati waendeshaji magari wamekuwa wakisaidia kupeleka wagonjwa hospitalini, haswa nyakati za usiku sisi tutawasaidia wenye uhitaji kufika vituoni kupiga kura.”

Rais na Rais mstaafu wamaliza tofauti zao
Katibu Mkuu atunukiwa uraia wa heshima Japan