Dhoruba ya mgogoro wa uenyekiti inazidi kuipasua mashua ya Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya chama hicho kutofautiana.

Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya udhamini ya chama hicho, Abdallah Khatau kutangaza kutomtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti au mwanachama wa chama hicho huku akiungwa mkono na wajumbe watatu wa Zanzibar, wajumbe watano wa bodi hiyo walioko Bara jana walijitokeza na kupinga msimamo huo.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wajumbe hao wa bara walisema kuwa wao hawakitambui kikao cha bodi hiyo kilichoitishwa na mwenyekiti wake na kwamba kinachofanyika ni muendelezo wa ‘Usulutani’ wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kutaka kuwatimua viongozi.

“Katibu amejifanya Sultani kwa muda mrefu. Amemfukuza maparara kiujanjaujanja, kamfukuza Hamad Rashid kiujanjaujanja, kamfukuza mwanzilishi wa chama hiki, Mussa Haji Kombo,” alisema mjumbe Shashu Lugeye.

Wajumbe hao watano kutoka Bara walikitupia lawama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo wakidai kuwa ndicho kinachochochea mgogoro huo na kwamba suluhu haikuwa kumfukuza Profesa Lipumba bali uongozi wa CUF kukaa meza moja kutafuta suluhu.

Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Joseph Mtatiro aliwaambia waandishi wa habari kuwa Profesa Lipumba anatumiwa na Chama Cha Mapinduzi kukipasua chama hicho.

Juzi, vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao CUF ni mdau, vilitangaza rasmi kutomtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti mwenza wa Umoja huo kwani alikikimbia chama chake wakati wa mapambano (uchaguzi) na kwamba ameona hakijaanguka kama alivyotarajia na sasa amerejea.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho akipinga uamuzi wa kumpokea Edward Lowassa (mgombea wa Chadema) na kumpa nafasi ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka jana akiungwa mkono na Ukawa.

Hata hivyo, mwaka huu Profesa Lipumba aliandika barua ya kutengua tena uamuzi wake wa kujiuzulu na kurejea kwenye nafasi yake ya Uenyekiti.

TCRA yafungia Kipindi cha Clouds TV kwa kuhamasisha ukahaba
Video: Taarifa ya jengo la TPA, jengo refu zaidi Afrika Mashariki na Kati