Serikali imepongeza juhudi za wadau wa Tasnia ya Filamu nchini kutokana na jitihada zao katika kuhakikisha tasnia hiyo inakuwa na kuwaletea maendeleo endelevu ikiwemo Ajira za uhakika kwa vijana.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania (KBF) Bibi. Joyce Fissoo alipokutana na ujumbe kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya TYEOO walipo mtembelea ofisini kwake jana kwa ajili ya kutambulisha rasmi Mradi wa TYEEO Barazani entertainment jana Jini Dar es Salaam.

Fissoo alisema kuwa mradi huo ni muhimu kwa mustakabari wa kukuza tasnia ya Filamu nchini kwani utarahisha kufikisha katika kuwafikia wadau wengi zaidi wa tasnia hiyo walioko katika mikoa ya pembezoni.

“Niseme tu kwa dhati kabisa nawapongeza sana kwa ubunifu wenu mradi huu ni mzuri na utaongeza tija katika tasnia yetu ya Filamu, nami ninawaahidi kuwapa ushirikiano pindi mtakapo kuwa mnanihitaji”. Alisema Fissoo.

Aidha alitoa ushauri kwa Taasisi hiyo kutumia vibanda vya maonyesho ya Filamu vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kutekeleza mradi huo kwa kuwa nia ya Serikali ni kuona dhana ya urathimishaji wa kazi za wasanii inafanikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TYEEO, John Kallaghe amesema kuwa pamoja na kuwa mradi huo ni binafsi lakini kutokana na imani kubwa walionayo juu ya Bodi ya Filamu wameona siyo busara kuendelea kutekeleza jambo kubwa kama hili bila ya kushirikisha mamlaka hiyo ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa Tasnia ya Filamu nchini.

Aliongeza kuwa wazo la kuanzishwa kwa mradi huu lilikuwa ni kusaidia kuwawezesha vijana kujikomboa katika lindi la umaskini kupitia huduma itokanayo na mradi huu ambayo ni utayarishaji na usambazaji wa kazi za wasanii wa Filamu kwa njia ya kisasa zaidi.

Kallaghe alisema kuwa wao kama wadau tasnia hiyo wako tayari kupokea ushauri na maelekezo ya namna ambavyo wanaweza kuboresha na kutekeleza mradi huo kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Mradi wa TYEEO Barazani ni miongoni mwa miradi kadhaa ambayo imeanzishwa na taasisi ya TYEEO, ulioasisiwa tangu mwaka 2013 na unakadiriwa kutoa fursa ya ajira za uhakika kwa vijana takribani 6000  katika kada zote za Filamu hadi kufikia mwaka 2017.

Naj 'amshindwa' Baraka Da Prince, amsaka mwalimu wa Kiingereza
Video: Mrema awageukia wanaopinga Serikali kuhamia Dodoma