Klabu ya Simba huenda ikaadhibiwa kwa kosa la kugomea kuvaa medali za mshindi wa pili wa ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2016/17.

Afisa mtendaji mkuu wa bodi ya ligi, Boniface Wambura amesema tayari ameshauandikia barua uongozi wa klabu hiyo kongwe hapa nchini, ili kupata maelezo ya kina, kwa nini kikosi chao kiligomea kuvalishwa medali mara baada ya mchezo wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Mwadui FC.

Wambura amesema kilichofanywa na viongozi na wachezaji wa klabu ya Simba sio kitendo cha kiungwana na wala hakiendani na tamaduni za mchezo wa soka popote pale duniani.

“Tumewaandikia kwa kutaka kujua sababu za msingi kwa nini walikataa kuvishwa medali mara baada ya mchezo wao wa mwisho wa ligi dhidi ya Mwadui FC, na ilithibitika wao ndio washindi wa pili katika ligi ya msimu uliopita,”

“Kama tutajiridhisha kwa sababu watakazotupa kwa njia ya maandishi, na tukaona walikua wana haki ya kimsingi ya kutovalishwa zile medali, tutaangalia mambo mengine, lakini wakishindwa kutupa sababu za msingi tutatumia taratibu za kinidhamu kuwaadhibu.” Amesema Wambura

Hata hivyo Wambura amesema katika barua waliouandikia uongozi wa klabu ya Simba, pia wametaka waelezwe sababu za kushindwa kufika katika hafla ya utoaji wa tuzo iliyokua imeandaliwa na mdhamini mkuu wa ligi ya Tanzania bara.

Simba hawakufika katika hafla hiyo, licha ya baadhi ya tuzo kwenda kwa wachezaji wao akiwepo Mohamed Hussein aliyetangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu na Shiza Kichuya aliyepata tuzo ya goli bora la msimu.

Kizungumkuti Chatawala Kambi Ya timu Ya Taifa Ya Ngumi
Akamatwa kwa kumshawishi mpenzi wake ajiue kisha achangishe fedha mtandaoni